Na Gideon Gregory,Dodoma
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Methew amesema utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rorya-Tarime kwa kutumia chanzo cha maji ya Ziwa Victoria umefikia wastani wa asilimia 12.5 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2025 ambapo utanufaisha watu 460,885 waishio kwenye Wilaya za Rorya, Tarime pamoja na Mji wa Sirari.
Naibu Waziri Kundo ameyasema hayo leo Juni 7,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Rorya Jafari Chege aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 utaanza kutekelezwa katika Wilaya ya Rorya.
“Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) yenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku, ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji (water treatment plant) yenye uwezo wa kutibu maji lita milioni 28 kwa siku, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 110, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster station) pamoja na ujenzi wa matanki matatu (3) yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 10”,amesema Mh.Kundo.