Na Costantine James,Geita
Wachimbaji wadogo wa madini wawili wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha mchanga wakati wakiendesha Shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika eneo lisilo rasmi kwa uchimbaji katika kijiji cha Magenge Kata ya Magenge wilayani Geita.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita Wambura Fidel amesema tukio hilo limetokea Juni 5, 2024 na kubainisha kwamba baada ya kupata taarifa za tukio hilo walifika eneo la tukio na kuanza shughuli za Uokoaji kabla ya kufanikiwa kupata miili ya watu hao wawili.
Baadhi ya mashuhuda wamesema walipata taarifa za tukio hilo Juni 5, 2024 na kuanza jitihada za uokoaji katika eneo hilo ambalo licha ya serikali ya Kijiji kupiga marufuku uchimbaji, baadhi ya watu wamekuwa wakiendesha shughuli hizo kimya kimya.
Diwani wa Kata ya Magenge Edward Fujo amesema moja ya sababu kubwa iliyopelekea kutokea kwa tukio hilo ni kufanyika kwa uchimbaji kwa njia zisizo rasmi katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuwataka wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini kutoa taarifa kwa serikali za mitaa kuhusiana na maeneo ya uchimbaji wanayoyamiliki hatua itakayoasaidia kuimarisha ulinzi hatua itakayosaidia kupunguza matukio ya ajali za mara kwa mara.