Mtu mmoja ameuawa na wengine nane kujeruhiwa usiku wa kuamkia leo kufuatia mlipuko katika kituo kimoja cha jeshi la Iraq, ambacho kinatumiwa na muungano wa makundi yenye silaha yanayoiunga mkono Iran.
Mlipuko huo ulitokea kwenye kituo cha jeshi cha Kalsu katika jimbo la Babylon lililo kusini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambako kuna vikosi vya muungano wa Hashed al-Shaabi na umetokea siku kadhaa baada ya Iran kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Kitengo cha habari cha jeshi la Iraq kilisema mlipuko na moto vililipiga kituo cha Kalsu alfajiri ya ya leo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi wanane na Muda mfupi baada ya mlipuko huo,jeshi la Marekani limesema vikosi vyake havihusi katika shambulio hilo.
Kundi la Hashed al-Shaabi kupitia taarifa yake limesema kwamba mlipuko huoumesababisha hasara kwa watu na mali bila kufafanuwa zaidi, ingawa lilikiri kuwa majengo yake kwenye kituo hicho cha kijeshi yameshambuliwa na kwamba wachunguzi wametumwa kwenye eneo hilo.