Viongozi G7 kuichukulia hatua Iran

Viongozi wa nchi saba tajiri duniani – G7 wameonyesha uungaji mkono wao kamili kwa Israel kufuatia shambulizi la Iran na kusema wako tayari kuchukua hatua zaidi katika kujibu walichoita mipango zaidi ya kuyumbisha kanda.


Katika taarifa kufuatia mkutano wa video, viongozi hao wa G7 wamesema wanalaani vikali shambulizi la moja kwa moja na lisilo la kawaida la Iran dhidi ya Israel na kuitaka Iran na washirika wake kusitisha mashambulizi yao.


Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema katika taarifa tofauti kuwa watatafakari vikwazo zaidi dhidi ya Iran kwa ushirikiano wa karibu na washirika wao, na hasa kuhusu mipango ya nchi hiyo ya matumizi ya droni na makombora.


Iran ilifanya shambulizi, lake la kwanza la moja kwa moja kwenye ardhi ya Israel ikiwa ni sehemu ya kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi kali la angani lililodaiwa kufanywa na Israel na kuharibu jengo la ubalozi wake mdogo katika mji mkuu wa Syria Damascus mapema mwezi huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *