ZUIO LA VIONGOZI ANGOLA: ACT WAZALENDO WATAKA MSIMAMO WA SERIKALI

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kufafanua tukio la kuzuiliwa kwa Viongozi lililotokea nchini Angola na msimamo wa Serikali juu ya suala hilo.

Tamko hilo limekuja baada ya viongozi wa vyama mbalimbali kuzuiliwa kuingia jijini Luanda kwa ajili ya kushiriki mkutano kuhusu masuala ya demokrasia akiwemo kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu.

Wengine waliozuiliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud.

Mara baada ya tukio hilo, Lissu alichapisha kwenye ukurasa wake wa X kuwa Mamlaka za uhamiaji za Angola ziliwazuia na kukataa kuwaruhusu kuingia nchini humo, yeye pamoja na ujumbe wa zaidi ya Viongozi Wakuu 20 na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa kutoka Kusini mwa Afrika.

Lissu aliandika kuwa, “ambao tuliwasili Luanda mapema leo kwa ajili ya mkutano huo wa siku mbili, kundi hili linajumuisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa kutoka Tanzania (0thman), Rais wa zamani wa Botswana, Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho, pamoja na viongozi na wajumbe waandamizi kutoka Kenya, Sudan, Tanzania, Afrika Kusini, Namibia, Eswatini, Lesotho, Ujerumani, Marekani, Uganda, DRC, na Msumbiji.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *