ZITTO KABWE AMJIBU GAMBO, AMTAKA AHUDHURIE VIKAO….

Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, amemjibu Mrisho Gambo kwa kumwambia vikao vya Kamati ya Fedha na Mipango vya Manispaa, Baraza la Madiwani na Baraza la Ushauri Mkoa (RCC) ni vikao vya kisheria.

Kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, Zitto amejibu habari yenye utetezi wa Gambo akiandika “Lakini Mrisho, vikao vya Kamati ya Fedha na Mipango vya Manispaa, Baraza la Madiwani na Baraza la Ushauri Mkoa (RCC) ni vikao vya kisheria, Wabunge wengi haswa wa siku hizi mnadharau sana vikao vya chini na matokeo yake hamfanyi kazi ya uwakilishi vizuri, huu utetezi wako sio”

Zitto amejibu pia hoja ya Mdau wa Mtandao huo aliyeandika Wabunge wengi wanajisahau kutokana na kupita bila kupingwa maana wanaamini Chama dola kitawabeba na laiti kungekuwa na ushindani wa kweli kwenye sanduku la kura wasingekuwa Wazembe……….. Zitto akaandika “Sio kujisahau, Wabunge wengi wanadharau vikao vya chini, nilipokuwa Mbunge moja ya vikao nilikuwa nahakikisha sikosi ni RCC, hiki ni kikao ambacho kinakupa sura ya maendeleo ya Mkoa mzima, kuna nyakati kikao kizima nilikuwa Mbunge pekee yangu kati ya Wabunge 8 wa Mkoa” – Zitto Kabwe.

Utetezi wa Mbunge wa Arusha, Mrisho Gambo umekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kumtaka Gambo kuachana na siasa za uchonganishi na badala yake ahudhurie vikao vya mipango ngazi ya Halmashauri na vya ngazi ya Mkoa ili kujadili pamoja kuhusu changamoto na suluhu za masuala mbalimbali yanayohusu Mkoa wa Arusha. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *