Na Saulo Steven – Singida.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Singida linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza majanga ya moto na kulinda mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, Mrakibu Debora Bigawa amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mbinu bora za kujikinga na moto, hasa majumbani.
“Tunaendelea na kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama gesi na majiko bora, ambayo siyo tu yanapunguza matumizi ya kuni na mkaa, bali pia hupunguza hatari ya moto,” amesema Bigawa.

Ameongeza kuwa hali ya usalama wa moto mkoani Singida kwa sasa ni ya kuridhisha, kwani hakuna matukio makubwa yaliyoripotiwa katika kipindi cha hivi karibuni,
“Tunaendelea kuhimiza tahadhari. Wananchi wanapaswa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na maarifa ya msingi ya hatua za kuchukua pindi ajali za moto zinapotokea,” amesema.
Jeshi hilo limeeleza kuwa litaendeleza kampeni hiyo kupitia shule, taasisi, na mikusanyiko ya kijamii ili kuhakikisha elimu hiyo inamfikia kila mmoja, hususan maeneo ya vijijini ambako uelewa bado ni mdogo.