ZIMAMOTO SIMIYU LADHIBITI WANANCHI KUCHOTA MAFUTA KWENYE LORI LA AJALI…

Na SAADA ALMASI -SIMIYU


Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Simiyu limefanikiwa kudhibiti wananchi waliojitokeza kuchota mafuta katika eneo la Njia panda Kata ya Isenga wilayani Maswa mkoani Simiyu mara baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kupata ajali na kupinduka.

Lori hilo lililokuwa na kichwa chenye namba za usajili T 524 DUD na tanki lenye namba za usajili T 702 DDZ mali ya kampuni ya PKM Limited lilikuwa likitokea jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Mara lililokuwa likiendeshwa na dereva Khalid Khassim (34).

Lori hilo lilipata hitilafu iliyosababisha kudondoka eneo hilo ndipo
wananchi wa maeneo hayo waliamua kujitokeza kutumia fursa hiyo kuanza kuchota mafuta.

Akitoa taarifa baada ya udhibiti huo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu Faustine Mtitu amewataka wananchi kutojihatarishia Maisha yao kwa kuendelea kuwa na tabia ya kuchota mafuta pindi ajali inapo tokea kwani hatari yake ni kubwa.


“Hiki kitendo kinatoa hatari barabarani na kuisogeza nyumbani mafuta uliyochukua yanaweza kuwa na faida ya shilingi elfu 50 ukiyauza lakini unakwenda ukayatunza kwenye nyumba ya thamani ya shilingi
milioni 20 yakilipuka umepata hasara zaidi” -Kamanda Mtitu.


Aidha kamanda mtitu amewataka wale ambao hawajasalimisha mafuta hayo kwa hiyari ikiwa ni pamoja na wale walioyapeleka katika mashamba yao kujitokeza na kusalimisha kabla vyombo vya sheria havijachukua
mkondo wake.


“Tumetoa elimu na walioelewa wamesalimisha ila wapo ambao wameyapeleka mashambani sisi tunawaachia jeshi la polisi watawasaka na hapo shEria itachukua mkondo wake” – Kamanda Mtitu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *