Faustine Kasala – Kigoma.
Jeshi la Zima moto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma limefanya zoezi la utayari wa kukabiliana na majanga ya moto katika soko la Kigoma Mjini kwa lengo la kuikumbusha na kuiandaa jamii namna ya kujiokoa na kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Mrakibu Msaidizi na Kaimu kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma Michael Maganga amesema Jamii inapaswa kuchukua tahadhari ya namna ya kujiokoa hususani inapotokea mlipukowa moto katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi.

”Moto huu ambao mmeushuhudia ni wakupangwa kwa lengo la kutoa elimu kwenu ninyi wananchi ili inapotokea changamoto ya moto sehemu yoyote ile muwe na uelewa wa namna ya kukabiliana na moto huo na namna ya kujiokoa” alisema Maganga.
Aidha amesema Miundombinu ya Soko hilo siyo rafiki katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo pindi mlipuko wa moto ukitokea na kwamba Jeshi hilo lilikwisha toa maelekezo kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya soko hilo kushughulikia changamoto hizo ikiwemo uwepo wa njia zinazoweza kuruhusu kuingia kwa magari ya zimamoto maelekezo ambayo hadi sasa hayajatekelezwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma Juma Rashidi Chaurembo amesema ni kweli Soko hilo linakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa njia kuu zinazoruhusu kuingia magari ya Zimamoto ndani ya soko jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na mali zao.
”Unajua Soko letu hili awali kulikuwepo na milango mikubwa ambayo ilikuwa inaruhusu magari ya zima moto kuingia ndani ya soko ili kukabiliana na mlipuko wa moto lakini kwa sasa milango hiyo imeendelea kupunguzwa kwa kuuzwa na kukodishwa na watu wa Manispaa hatimaye njia hizo sasa hazipo jambo ambalo ni hatari endapo mlipuko wa moto ukitokea.” Alisema Chaurembo.

Chaurembo amesema maelekezo mengine waliyopokea kutoka katika Jeshi hilo wanaendelea kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa vya kuzimia moto (Fire Extinguishers), vinakuwepo, mama lishe kuhakikisha wamezima moto na kusafisha pindi wanapofunga biashara zao.



