ZIFAHAMU PESA ZILIZOKUSANYA NA TRA KWENYE ROBO YA PILI YA MWAKA WA FEDHA 2024/25……

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25 imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh.Trilioni 8.741 sawa na ufanisi wa asilimia 104.63 ya lengo la kukusanya sh.Trilioni 8.356 ya ukuaji wa asilimia  19.05 ukilinganisha na kiasi cha sh.Trilioni 7.342 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Huku katika robo hiyo ya pili ya mwaka 2023/24 TRA imevunja rekodi ya makusanyo kwa mwezi Desemba 2024 kuweza kukusanya kiasi cha Sh.Trilion 3.587 ambacho ni kiwango cha juu katika ukusanyaji wa kodi kwa mwezi mmoja toka TRA kuanzishwa kwake.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa TRA,Yusuph Mwenda wakati akiongea na waandishi wa habari alisema makusanyo hayo yaliyofanywa katika kipindi hicho yanapelekea TRA kuwa imekusanya kiasi cha sh.Trilioni 16.528 katika nusu ya kwanza (Julai -Disemba 2024) ya mwaka wa fedha 2024/25.

Alisema TRA pia imeandika rekodi mpya ya kuweza kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi sita mfululizo katika nusu ya kwanza Julai -Disemba ya mwaka  wa fedha 2024 /25.

Kamishna Mwenda alisema wastani wa kiwango cha makusanyo kwa mwezi umeongezeka kwa asilimia 18.80 toka wastani wa sh.trilioni 2.319 kwa mwaka wa fedha 2023/24 mpaka kufikia wastani wa Sh.Trilioni 2.755 kwa mwezi,mwaka huu wa fedha.

“Ufanisi huu  katika makusanyo uliofikiwa mwezi  Julai -Desemba  mwaka wa fedha 2024/25 kwa kiwango kikubwa umechangiwa na kuendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika maeneo ambayo TRA imeweka Mkazo ikiwemo kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchinikwa kushirikiana na walipakodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto za walipakodi wote nchini,” alisema Kamishna Mwenda. 

Alisema pia kuongezeka kwa utendaji kazi mzuri,nidhamu na ubunifu kazini kwa watumishi wote  wa TRA nao ni mchango wa kupaa kwa mapato hayo.

“Ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa miezi ya Julai hadi Disemba mwaka wa fedha 224/25 ni kiashiria chanya katika kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka  2024/25 la sh.Trilioni 30.04 yanafikiwa.

“Katika kufanikisha hili katika miezi iliyobakibya mwaka wa fedha 2024/25 menejimenti ya TRA inaendelea kutekeleza kikamilifu mambo mbalimbali ikiwemo maagizo ya Rais Samia  kuhusu usimamizi wa kodi nchini  kwa hiari na kuanza matumizi ya mfumo wa usimamizi wa forodha (TANCIS) ulioboreshwa na mfumo wa usimamizi wa kodi za ndani (IDRAS) kuanzia mwezi wa Januari 2025,”alisisitiza. 

Aidha alisema TRA itaendelea kuimarisha usimamizi wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD nchini kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji pamoja na kuwakumusha wananchi juu ya umuhimu wa utoaji wa risiti hizo .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *