Leo Novemba 17, 2023 ni siku ya mtoto njiti duniani ambayo inaadhimishwa kwa lengo la kutoa elimu kuhusu watoto njiti ambao wanazaliwa kabla ya muda sahihi kukamilika wakiwa hawajakomaa na kufikisha wiki 37 pamoja na kutambua na kuthamini uwepo na umuhimu wao kama walivyo watoto wengine.
Katika mkoa wa Shinyanga takwimu zinaonesha kuwa kwa mwezi watoto njiti zaidi ya 30 wanapokelewa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wengi wao wakiwa ni watoto mapacha sababu ikielezwa kuwa ni pressure za ujauzito na uhudhuriaji hafifu wa kliniki kwa mama wajawazito.
Mkuu wa idara ya watoto kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dokta Allon Mwamfula ameeleza hayo leo wakati akizungumza na Jambo FM na kuongeza kuwa kwa sasa vifo vya watoto hao vimepungua iikilinganishwa na hapo awali kutokana na huduma na vifaa tiba vya kisasa vilivyopo hospitalini hapo.
Aidha dokta Mwamfula amewasihi wanawake wajawazito na wanaotarajia kuwa wajawazito kuwa na desturi ya kuhudhuria mapema kliniki mara baada ya kugundua ni mjamzito ili kupunguza na hata kuondokana na changamoto ya mtoto njiti nchini.