ZAIDI YA WANAFUNZI 1500 MKOANI MARA WASOMA KWA KUPOKEZANA KISA HIKI HAPA…

Adam Msafiri, Bunda, Mara.

Zaidi ya wanafunzi 1,500 katika shule za msingi Salama A na Salama B wilayani Bunda mkoani Mara, wamejikuta wakilazimika kuhudhuria vipindi vya masomo shule kwa kupokezana kufuatia changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hizo mbili zilizopo katika eneo moja.

Mmoja wa wanafunzi wanaosoma katika  shule hizo, Yusuf John amesema wanapata changamoto katika kujifunza na kwamba hali hiyo imefanya baadhi ya wanafunzi wenzake kufika shule kwa kusuasua huku akitoa wito kwa jamii,wadau na serikali kuingilia kati ili kuwakwamua na changamoto hiyo.

‘‘Wanafunzi wengine wanakua watoro,unakuta wanakuja leo,kesho hawaji,kesho kuwa wanakuja yaani hivyo hivyo,madarasa yakiwepo tutafaulu sana’’ Amesema Yusuf ambaye ni mwanafunzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Salama A,eneo ambalo shule hizo zinapatikana Bw.Michael Mbata,anakiri kuwa shule hizo zina uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo ameeleza kuwa mtindo wa watoto wao kusoma kwa kupokezana madarasa una hatarisha maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi. 

Akielezea hali halisi ya mambo ilivyo, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Salama A,Lucas Karebu anabainisha kwamba wamelazimika kupanga ratiba ya wanafunzi kuhudhuria vipindi kwa zamu kutokana na ukosefu wa madarasa na kwamba kwa sasa kumeanza kukithiri hali ya utoro kwa wanafunzi inayochangiwa na adha hiyo.

Mwalimu Karebu amesema‘Kuna changamoto watoto kusoma kwa shift,ambapo sasa shule moja inaingia saa moja na nusu ambapo saa sita na nusu inakuwa mwisho wa shift ya asubuhi,watoto wanaoingia shift ya mchana wanashindwa kufika vyema shuleni pengine kutokana na kuwa na jua kali ama sababu nyingine.’’

Kwa kuliona hilo, tayari Benki ya Nmb imeguswa na changamoto hiyo ambapo Kaimu Meneja wa Nmb kanda ya Ziwa Humphrey Kaaya amesema wamechangia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 ili kuzisaidia shule hizo ambazo kwa sasa zinahitaji vyumba vya madarasa 19 ili kuondokana na uhaba wa madarasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *