Na Saada Almasi – Simiyu.
Zaidi ya viongozi 50 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka katika mikoa inayounda kanda ya Serengeti yaani Shinyanga,Simyu na Mara wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa kanda hiyo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho wilayani Itilima mkoani Simiyu Jakson Scania Luyombya wamekutana wilayani ariadi mkoani simiyu na kutoa azma yao ya kujivua uanachama wa chama hicho kwa kile wanachodai kuwa kumekuwa na lugha za matusi, kejeli na kukosa muelekeo hasa kwa kujitoa kwake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Viongozi wengine waliojivua ni pamoja na Amos Sobanja aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wazee mkoa wa Simiyu, Tatu Isole mweka hazina Mkoa wa Simiyu, Kwandu Mpanduzi mjumbe, Nkuba Daudi wakala wa usajili kidijitali Wilaya ya Maswa na Steven Kitama Mkufunzi wa chama hicho ikiwa ni siku moja tangu kufanyika kwa mkutano wa chama hicho mkoani humo katika muendelezo wa kupita mkoa kwa mkoa kueleza kampeni ya No Reform No Election na Tone Tone.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Jakson Scania amesema kuwa tangu kufanyike uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti wa chama hicho kumekuwa na mpasuko wa makundi mawili Freeman Mbowe na Tundu Lisu ambayo kila kundi likimtuhumu mwezie kwa maneno makali na kejeli.
“Chama chetu kimekuwa na magenge mawili tangu kufanyika kwa uchaguzi mwezi Januari mwisho wa siku kumekuwa na kurushiana maneno na migogoro kutoelewana na kupasuka kati ya kundi la Mbowe na Tundu Lisu sasa sisi tulio muamini Mbowe tumekuwa hatuko huru kufanya siasa tuna hofu mara kuondolewa uanachama “ amesema Scania.
“Kule tuendako mbele ya safari siioni asubuhi yetu naona giza tu mimi mwenyewe nimekuwa mtu wa kubezwa kudharauliwa na kutukanwa na Watoto wadogo sasa sioni haja ya kuendelea na siasa bora nitafute kitu kingine cha kufanya,” alisema Amos Sobanja.
Awali akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani humo katibu wa chama hicho Taifa John Mnyika ametoa maelekezo kwa mwanachama yeyote mwenye nia ya kuhama chama hicho awe huru kuhama na wanaobaki wazibe nafasi zilizoachwa ili kuendelea na azma ya No Reform No Election.
“Ikitokea mtu yeyote amesaliti amehamia chama tawala ama chama chochote cha siasa basi nafasi yake izibwe kwa kuingiza wanachama wapya na tuendelee kulisukuma gurudumuletu la No Reform No Election kwa sababu tunahitaji mabadiliko,” alisema Katibu Mnyika.