Zaidi ya pikipiki 100 hukamatwa kila siku kwa uvunjaji wa sheria barabarani – Kahama

Zaidi ya pikipiki 100 za magurudumu mawili maarufu bodaboda zinakamatwa kila siku na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kwa kuvunja sheria Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga kufuatia zoezi la kukamata wavunja sheria za usalama barabarani lilionza Septemba 6 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Usalama Barabarani Manispaa ya Kahama ACP Frola Nangawe wakati wa mahojianop maalumu na Jambo FM.

“Pikipiki ni nyingi kwasababu tumekuwa tukikamata katika siku tofauti tofauti,kwa siku tunakamata zaidi ya pikipiki 100 na wakati mwingine tunaweza kukamata pikipiki 65 na tunaendelea kutoa elimu kwenye vijiwe vya bodaboda”

Katika hatua nyingine ACP Nangawe ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya moto kukata bima ya vyombo vyao ili inapotokea ajali iwe rahisi kufuatilia fidia na kuwataka watumiaji wa vyombo hivyo vya moto kuegesha magari sehemu sahihi hali itakayosaidia kupunguza msongamano na ajali za barabarani.

Nao baadhi ya wananchi wa manispaa ya Kahama wamelipongeza jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani kwa zoezi hilo la kuwakamata madereva wanaovunja sheria na kuomba zoezi hilo kuwa endelevu huku wakiwataka waendesha vyombo vya moto Kwenda kwenye vyuo vya udereva kusomea fani hiyo na kujua sheria za barabarani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *