Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Zaidi ya bilioni 101.2 kujenga barabara ya Kahama-Kakola km 73 kwa kiwango cha lami

Serikali imesaini Mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kahama-Bulyanhulu Jct – Kakola (km 73) kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa za kiuchumi za madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.

Mkataba huo umesainiwa kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa gharama ya Shilingi Bilioni 101.2 kwa ufadhili wa Kampuni ya Madini
ya Barrick Tanzania Mining Companies (BTMCs) na Serikali ya Tanzania.

Akishuhudia Utiaji Saini wa barabara hiyo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa barabara hii imekuwa ni kilio cha muda mrefu na sasa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri na wawekezaji wa ndani ya nchi ikiwemo kampuni ya Barick ametoa kibali barabara hiyo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Mohamed Besta ameeleza kuwa Mkandarasi aliyeshinda zabuni ni Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa muda wa Miezi 27 na kusimamiwa na TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU).

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Rais pia ameelekeza Wizara ya Ujenzi kuanza hatua za kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Iloginhadi Mtakuja (km 57.4) ambayo ni barabara ya kiuchumi na inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Geita.

Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Mijini (TARURA) kuona namna ya kuboresha miundombinu ya barabara za Mji wa Kahama ili kuusaidia mji huo katika ukuaji wake wa Kiuchumi na kijamii.

Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa mtandao wa barabara kwa zile za changarawe na zile za lami zilizopo Mkoani Shinyanga zitaendelea kusimamiwa na kuhudumiwa ili ziweze kupitika msimu wa kiangazi na vuli ikiwemo barabara ya Old Shinyanga – Solwa – Burige mpaka Kahama pamoja na ile Kolandoto-Lalago.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *