Zaidi ya 4,900 wabainikia kuwa na Kifafa Geita

Mkoa wa Geita unakabiliwa na changamoto ya uwepo wa watu wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kifafa kwa watu wazima na watoto katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kutokana na ugonjwa husika kutokupewa kipaumbele zaidi katika jamii na sehemu za kutolea huduma za matibabu hasa katika Zahanati na Vituo vya Afya.

Hayo yamebainishwa leo Mei 6,2024 na Mratibu wa Afya ya akili mkoa wa Geita Alfredina Fredrick wakati akizungumza katika mafunzo ya kifafa, tiba na jinsi ya kumtambua mgonjwa kwa waratibu wa afya ya akili,magonjwa yasiyoambukiza ngazi ya wilaya na watoa huduma yaliyofanyika mjini Geita ambapo amesema ugonjwa huo upo juu zaidi kwa magonjwa yasiyoambukiza kwa Mkoa wa Geita kwani kuanzia  2022 hadi Machi 2024 watu zaidi ya 4,900 wamebainika kuwa na ugonjwa huo.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dr. Omary Sukari amewataka waratibu kwenda kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya ugonjwa wa kifafa pamoja na kuibua wagonjwa wapya ndani ya Jamii ili waanze kupatiwa matibabu kwa lengo la kupunguza changamoto ya ugonjwa huo kwa mkoa wa Geita.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema licha ya ugonjwa huo mara nyingi kuwa wa kurithi na uwepo wa sababu nyingine za kitalam zinazosababisha ugonjwa huo bado jamii inaamini kuwa ugonjwa huo ni laana au kurogwa hivyo wao kama waratibu watatumia elimu waliyoipata katika mafunzo hayo kwenda kutoa elimu kwa wananchi na kuwaibua wagonjwa waliopo katika maeneo yao yakazi ili waweze kupatiwa matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *