Wananchi wa Kata ya Mienze, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, wamepata afueni kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Idekamiso, mradi uliotekelezwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.
Kwa zaidi ya miaka 20, wakazi wa eneo hilo walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hali iliyosababisha baadhi ya wajawazito kushindwa kupata huduma muhimu kwa wakati.

Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza rasmi Septemba 4, 2023, ambapo wananchi walichangia fedha, vifaa na nguvu kazi hadi kufikia hatua ya boma kabla ya kukamilishwa.
Akizungumza katika hafla ya kukamilika kwa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mohamed Mtulyakwaku, amewahimiza wananchi kuitumia kikamilifu zahanati hiyo ili kuboresha afya zao.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na huduma ya bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha wanapata matibabu kwa urahisi na gharama nafuu.
Kukamilika kwa zahanati hiyo kunatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hususan kwa akina mama na watoto katika eneo hilo.



