Na Paschal Tuliano – Tabora
Mwanamke Mmoja aliyejulikana kwa jina la Chatherine Innocent Petro (21) mkazi wa eneo la Umanda kata ya Kalunde Manispaa ya Tabora amejiua kwa kunywa dawa ya kuulia wadudu.
Akithibitisha kutokea kwa tukio Hilo kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Tabora SACP Richard Abwao amesema chanzo cha tukio hilo inaelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi kutokana na migogoro ya kifamilia iliyokuwepo kati ya mwanamke huyo na mume wake.

“Ilipofika tarehe 14 majira saa 4 za usiku, mume aliporudi nyumbani alimkuta mke akigaragara nje ya nyumba yao huku akitapika ndipo alipomuuliza tatizo nini akamjibu amekunywa dawa ya kuulia wadudu.
Mgonjwa huyo alipatiwa huduma katika Zahanati ya Umanda na kupewa rufaa kwenda hospitali lakini hawakumpeleka badala yake wakamrudisha nyumbani, ndipo siku iliyofuata majira ya saa 12 jioni mwanamke huyo alifariki.” Ameeleza kamanda Richard Abwao.
Kamanda Abwao ametoa rai kwa wananchi hasa wanandoa kutokujichukulia sheria mikononi pindi wanapokuwa na migogoro ya kifamilia au migogoro mingine ndani ya jamii.
“Jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Tabora pale inapojitokeza migogoro ya kifamilia kutokujichukulia sheria mikononi ambapo ni kinyume na sheria ikiwemo kujiua kwa kujidhuru kama tulivyoshuhudia tukio hili.” Amesema Kamanda Abwao.
Mkoa wa Tabora unaendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa matukio ya mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi hapa nchini ambapo matukio ohayo yamekuwa yakiripotiwa kila uchwao.


