Na Melkizedeck Antony,Mwanza
Wananchi wa mkoani Mwanza wametakiwa kulinda miundombinu ya maji iliyopo katika maeneo yao ili miundombinu hiyo iwe endelevu kwa kizazi cha hapo baadae.
Rai hiyo imetolewa Septemba 04,2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Nelly Msuya wakati alipotembelea katika mradi wa dharura unaotoa maji katika eneo la Sawa kupeleka katika eneo la Buhongwa ambapo amesema katika kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa kata ya Lwanhima, Buhongwa na maeneo jirani serikali imeamua kujenga mradi huo wa maji hivyo ili mradi huo uwe endelevu kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu yake.
Msuya pia amesema mpaka sasa mradi huo umeshafikia asilimia 85 na wataendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuondoa kero ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake kaimu Meneja wa Kanda kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) Mhandisi David Katakweba amesema mradi wa dharura wa maji Buhongwa utakua ukichukua maji kutoka katika tanki la maji lililopo katika eneo la Sawa ambalo linauwezo wa kuzalisha kiwango cha lita laki nne kwa saa moja hivyo uwepo wa mradi huo utapunguza adha ya mgao wa maji uliopo katika eneo hilo.
Nae diwani wa kata ya Buhongwa Joseph Kabadi ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuanzisha mradi huo wa dharura kwani endapo utakamilika kwa wakati unakwenda kupunguza adha ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa kata ya Buhongwa, Lwanhima na maeneo jirani.