WITO: WATENDAJI, WADAU WAONGEZE NGUVU KUENDELEZA ELIMU YA WATU WAZIMA – DC WELLA

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewataka viongozi, watendaji na wadau wa elimu, kuongeza nguvu katika kuendeleza elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo yao.

Wito huo, ameutoa wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.

Amesema, shughuli za maadhimisho na uhamasishaji zinapaswa kushushwa hadi ngazi za Kata, kutokana na uwepo wa wananchi wengi wanaohitaji kupata elimu,maadhimisho haya yamefanyika viwanja vya shule ya Sekondari Uyui Manispaa ya Tabora. 

“Pelekeni maadhimisho haya ngazi za Kata kwa sababu ndio kuna watu wengi,” amesema Wella.

Katika kuimarisha mpango huo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu thamani na manufaa ya kusoma na kuandika, sambamba na kufanya utambuzi wa watu ambao bado wanahitaji kupata elimu ili waweze kufikiwa na huduma hizo. 

Amesema upatikanaji wa elimu kwa watu wazima unasaidia kuongeza maarifa na ujuzi unaomwezesha mwananchi kukabiliana na changamoto za maisha, kuimarisha maendeleo ya familia na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii. 

Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Kisomo kwa Manufaa ya Watu, Dunia na Ustawi wa Jamii,” yakilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi, pamoja na kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *