Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed amewataka Wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kutotengeneza makundi kati yao na kupigana vita, hali ambayo itasababisha kuvunjika kwa mshikamano baina yao.
Shemsa ameyasema hayo katika Baraza la Umoja huo lililoketi mjini Bariadi mkoani Simiyu, na kujumuisha ajenda mbalimbali kama elimu juu ya uchangiaji wa Bima za Afya na nafasi ya Mwanamke katika uongozi na kusema kuwa, Wanawake ni Jeshi kubwa ambalo likisimama kikamilifu, linauwezo wa kuwakomboa katika nyanja zote za maisha.
“Tumetoka katika kipindi cha uchaguzi na tumeona wenyewe ni namna gani wanawake tumechangia mwanzo hadi mwisho ,mimi ninaamini mwanamke ni jeshi ambalo likisimama hakuna jambo la maendeleo litakosa kusimama niwaombe mambo yaliyopita tusiyabebe, tusijenge matabaka, tusipigane vita wala kuchafuana sisi kwa sisi maana kabla hujaanza kumchafua mwenzio jua kuwa unaanza kuchafuka wewe,“ amesema Shemsa.

Ameongeza kuwa, “Mwanamke ni yule ambaye anaingia vitani na kupigana na katika hili niwapongeze wote mliothubutu kugombea nafasi mbali mbali za uongozi japo mpo mliopata nafasi na mliokosa huo ndio utimilifu wenu,na niwaambie CCM inautaratibu wake wa uongozi fursa zingine bado zipo mtagombea tena na nina imani mtashinda.”
Akitoa salamu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge amewaeleza Wanawake wa umoja huo kuwa Serikali imekuwa katika mapambano makubwa ya kuwafanya wanawake waondokane na mfumo kandamizi, ili kuwepo na usawa katika jamii.
“Mwanamke ukiacha kujitoa katika uongozi ama shughuli za kimaendeleo utakuwa haujitendei haki, kwa sababu siku zote serikali imekuwa ikipambania suala la usawa kati ya mwanamke na mwanaume na fursa tumepewa,”

“Kudhihirisha hilo Tanzania imeingia katika mikataba ya kimataifa ya kutokomeza hali za ubaguzi na bado mkataba wa Beijing uliotoa fursa ya viti maalum kwa wanawake, sasa kupitia hilo tambueni nafasi mmepewa mnatakiwa kuzitumia vizuri,” alifafanua Tina Chenge.
Kuhusu elimu ya Bima ya Afya kwa wote, Katibu wa UWT Wilaya ya Bariadi, Angel Simwanza amesema, hiyo ni moja ya ajenda muhimu ambazo Rais wa nchi ameahidi kutekeleza, hivyo kila Mwanamke anajukumu la kuhamasisha watu wanaomzunguka, ili kufanikisha malengo ya huduma bora za afya kwa Mtanzania.

“Kila mmoja wetu ana watu wake anaowaongoza tukawe mabalozi wazuri kufikisha elimu ya bima ya afya kwa wote kwani tunapochangia tunazadi kujenga mahusiano mazuri na upendo baina yetu bila kujali matabaka hata yule asiyekuwa na uwezo ataweza kupata huduma bora kwa sababu mimi na wewe tumechangia,” amesema Angel.
Naye Diwani Viti Maalum Wilaya ya Meatu, Zainab Abdallah amesisitiza umoja baina yao akisema, “wito wangu kwa wanawake wenzangu ni kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi na tusiogope kwani mifano ya viongozi wanawake tunayo basi na sisi tunaweza pia tudumu katika kushikana mikono na kutiana nguvu ili kwa pamoja tuvuke hatua moja kwenda nyingine.”

Kwa upande wake Mwakilishi toka Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu, Janeth Epafra amezungumzia fursa katika uchangiaji wa bima za afya, ili kuhakikisha kila mmoja anapata huduma zinazostahili bila vikwazo.
“Sisi kama viongozi tunapaswa kujua ni kaya ngapi ambazo hazijachangia kupata bima na zipi hazina uwezo na kuhamasisha ambao hawajachangia,hatua hiyi italeta urahisi kwa serikali kupata takwimu sahihi za wanufaika wa bima hizi na pia itakuwa rahisi kubaini sababi zinazomfanya mtu asichangie,” alisema Janeth.