WIKI YA UNYONYESHAJI MAZIWA YA MAMA YAZINDULIWA SINGIDA

Na Saulo Stephen – Singida.

Halmashauri ya Manispaa ya Singida, imezindua Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama kwa kutoa wito kwa akina mama kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa, ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa na kuhakikisha wanakuwa na afya bora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Singida, Dkt Lameck Isidory, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Bi Joanfaith Kataraia, alisema maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika kwa ukuaji na maendeleo ya mtoto katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa maisha.

Alisema unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni msingi wa afya ya mtoto, hivyo akina mama wanapaswa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya kwa kuwanyonyesha watoto wao mara tu wanapojifungua na kuendelea kwa miezi sita bila kuwapa chakula au kinywaji kingine isipokuwa pale wataalamu wa afya watakaposhauri vinginevyo.

Dkt. Isidory aliwataka pia waajiri, akina baba, watoa huduma za afya na jamii kwa ujumla kushiriki kulinda, kuhamasisha na kuthamini unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa kuhakikisha mazingira rafiki yanayowezesha akina mama kuwanyonyesha watoto wao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni mwanzo bora wa maisha ya mtoto.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Bi Dora Simon, alitoa elimu kuhusu sheria na haki zinazohusu unyonyeshaji wa mtoto pamoja na kusisitiza umuhimu wa malezi bora katika makuzi ya mtoto tangu anapozaliwa.

Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama huadhimishwa duniani kila mwaka kufuatia kuanzishwa mwaka 1991 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), ikiwa na lengo la kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya maisha ili kuboresha afya na kupunguza vifo vya watoto .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *