WHO Yavuka Lengo la Utoaji wa Chanjo ya Polio Gaza

Shirika la Afya Duniani (WHO) limefanikiwa kuvuka lengo la kuwapatia chanjo ya polio watoto kwenye Ukanda wa Gaza kuliko lililovyokuwa limetarajia kuwafikia katika awamu ya kwanza ya kampeni yake ya chanjo.

Katika awamu ya kwanza ya siku 10 iliyoanza Jumapili ya Septemba WHO limefanikiwa kugawa chanjo kwa zaidi ya watoto 161,000 kikiwa kiwango cha juu kabisa kwa siku mbili za mwanzo. 

Mwakilishi wa shirika hilo kwenye mamlaka za Palestina, Rik Peeperkorn akiwa Geneva,Uswisi amewaambia waandishi wa habari kwamba wanadhamiria kutoa chanjo kwa asilimia 90 ya watoto wa Gaza ili kuwaepusha na uwezekano wa kupatwa kwa maradhi ya polio ambayo yanaweza kusababisha ulemavu wa kudumu, kupooza na hata kifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Amebainisha kwamba lengo la WHO ni kuwachanja watoto 640,000 katika ukanda huo ambao eneo lake kubwa limegeuzwa kuwa vifusi, na sehemu kubwa ya wakazi wake milioni 2.4 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel na kukimbilia kwenye maeneo machafu, ambayo ugonjwa wa polio unahofiwa kuweza kusambaa kwa kasi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *