Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya Ukimwi duniani, Umoja wa Mataifa umesema bado inawezekana kufikisha mwisho janga hilo kufikia mwaka 2030, lakini endapo tu jamii za huduma mashinani zitawezeshwa.
Shirika la kupambana naUKIMWI la Umoja wa Mataifa, UNAIDS, lilisema katika Ripoti yake ya kila mwaka ya Siku ya UKIMWI Duniani kwamba majibu yanayoongozwa na jamii hayatambuliki, hayafadhiliwa ipasavyo na katika baadhi ya maeneo yanashambuliwa.
Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza uliweka lengo mwaka 2015 la kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo 2030.
Kuna watu milioni 39 duniani kote wanaoishi na VVU — virusi vinavyosababisha UKIMWI. Kati yao, milioni 20.8 wako mashariki na kusini mwa Afrika na milioni 6.5 wako Asia na Pasifiki, Lakini kati ya milioni 39, milioni 9.2 hawana matibabu ya kuokoa maisha.
Karibu dola bilioni 20.8 zilipatikana kwa ajili ya programu za VVU katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati mwaka 2022, hii ikiwa ni pungufu ya dola bilioni 29.3 zinazohitajika kufikia 2025.
Gharama ya kila mwaka ya matibabu imeshuka kutoka dola 25,000 kwa kila mtu mwaka 1995 hadi chini ya dola 70 katika nchi nyingi zilizoathiriwa zaidi na VVU siku hizi. Ripoti hiyo ilisema ufadhili unaopitishwa kupitia jamii umepungua kutoka asilimia 31 mwaka wa 2012 hadi asilimia 20 mwaka wa 2021.