NA EUNICE KANUMBA
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekabidhi kwa serikali ya Tanzania kituo cha Kimkakati kilichokuwa katika bandari ya nchi kavu Isaka wilaya Kahama mkoani Shinyanga lengo likiwa ni kugawa misaada ya chakula kwa wakimbizi waliokuwa wakitokea katika nchi za ukanda wa maziwa makuu kufuatia machafuko mbalimbali yaliyopelekea vita katika nchi za Burundi na Rwanda katika mwaka 1994.
Kituo hicho chenye eneo lenye ukubwa wa Mita za Mraba 29450 serikali iliwapatia WFP tangu Januari mwaka 1996 na mwaka 2004 ilithibitisha kwa barua kupokea kwake na mwaka 2024 imekabidhi kwa kurudisha rasmi eneo hilo kwa serikali.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Chakula duniani Christine Mendes amesema kituo hicho cha Isaka kilijengwa na shirika hilo kwa madhumumuni ya kusambaza chakula cha msaada kwa wakimbizi ambapo chakula hicho kilikuwa kikisafirishwa kutoka bandari ya Dar es salaam kupitia reli ya kati mpaka katika kituo hicho.
Mendes alisema chakula walichokuwa wakisambaza zaidi ni Maharage,Mahindi na Mtama na kwa kupitia na kupeleka kwenye nchi za Rwanda,Burundi,Kongo, Kenya ,Sudani Kusini na Uganda.
“Kituo hicho kilijengwa bure na WFP na kuweka mtandao wa miundombinu ya reli mbili za kutoka Stesheni ya Isaka hadi kwenye kambi hiyo yenye umbali wa mita 1200 waliweka Maghala 54 ya kuhamishika ,uzio,nyumba mbili za watumishi na Mashine “amesema Mendes.
Aidha Mendes ametoa mapendekezo kuwa eneo hilo wapatiwe Shirika la Reli (TRC) kwani shughuli walizokuwa wakizifanya wao zinaendana katika kutunza mizigo na usafirishaji.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika la reli Tanzania Meneja wa Shirika hilo kanda ya Tabora John Mamuya amesema wanashauri eneo hilo wapatiwe wao kwasababu hata katika ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) watalitumia kuhifadhi vifaa na ujenzi huo utakapokamilika litatumika kuweka mizigo inayotarajiwa kusafirishwa.
Naye Diwani wa kata ya Isaka Pazi Majuta amesema asilimia 70 ya uchumi wa Isaka ulijengwa na WFP na wao walikaa kwenye Halmashauri na kujadiliana kuhusu eneo hilo walipendekeza lilirudi kwenye kijiji ili waweze kuendeleza eneo hilo kwa kuweka miundombinu kama shule au kugawa maeneo.
Akitolea ufafanuzi mapendekezo ya wadau hao Katibu tawala wilaya ya Kahama Mohamed Mbega amesema ndio kwanza wamekabidhiwa eneo hilo hivyo mapendekezo yote yatajadiliwa katika vikao husika .