WENYEVITI WA MITAA BARIADI WATANGAZA KUJIUZULU WASIPORUDISHIWA MIHURI NDANI YA SIKU 30

Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.

Wenyeviti wa serikali za mitaa Mjini Bariadi mkoani Simiyu, wameipa Serikali siku 30, kuhakikisha wanarudisha mihuri katika himaya yao, ili waweze kuendelea na majukumu ya kuwatumikia wananchi kwa uhuru.

Wakiongea katika kikao cha pamoja kilichoketi mjini Bariadi, Wenyeviti hao wamesema kuwanyang’anya mihuri hiyo ni kuwanyima haki wananchi ya kuhudumiwa.

Wamesema, kumiliki mihuri hiyo na kuitiumia katika shughuli zao kunawapa urahisi wananchi kupata huduma ya mihuri pindi wanapokwenda kufuata huduma katika maeneo tofauti, zikiwemo taasisi mbalimbali za kiserikali na kutambulika bila tashwishi.

Baada ya kikao kumalizika na azimio kutolewa Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti hao, Mashaka Than amesema kutokuwa na mihuri hakuwapi uhuru wa kufanya kazi zao ukizingatia ndiyo serikali ya chini ambayo ipo karibu zaidi na wananchi kwa kusikiliza changamoto zao.

“Kila ambapo mwananchi anapohitaji huduma za serikali mara zote huanzia kwetu,tumekuwa tukihusika katika matukio mengi ,sasa kitendo cha kutokuwa na mihuri kinawezaje kutupa uhuru wa kazi zetu ili mwananchi adhihirike amepita kwetu? kwahiyo tunatoa hizi siku 30 kwa serikali  kuturudishia mihuri vinginevyo tunajiuzulu katika nafasi zetu,” amesema Mashaka Than.

Sambamba na hilo wenyeviti hao wameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda sheria inayoamuru wenyeviti wote wa seriakali za mitaa nchini kumiliki mihuri kisheria pasi na kubugudhiwa na mamlaka yoyote.

Itakumbukwa kuchukuliwa kwa mihuri kwa wenyeviti wa mitaa ilikuwa tukio la nchi nzima ambalo lilitokana na mabadiliko ya kiutendaji na maelekezo ya serikali kuanzia mwaka 2010 ambayo kwa kiasi kikubwa yalipunguza matumizi ya mihuri, ili kuzuia matumizi mabaya ya madaraka, kuimarisha mfumo rasmi ya utambulisho, kudhibiti urasimu pamoja na kuweka uwajibikaji kwenye watendaji wa serikali.

Hata hivyo kwa mujibu wa taratibu za kazi za Mwenyekiti wa Mtaa tangazo la serikali Na,3 la Tarehe 09/05/1994 linaeleza kuwa Mwenyekiti wa mtaa ama kijiji anatakiwa kuwa na Bendera yenye nembo yay a Halmashauri, Rejesta ya wakazi wote wa mtaa na Daftari la mihtasari ya vikao vya mtaa na si vinginevyo hivyo kufuatana  na hilo kumiliki mihuri si sahihi kwani hakuna kanuni wala Taratibu zinazoelekeza wenyeviti hao kuendelea kutumia mihuri bila ruhusa kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *