Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria kuhakikisha wanazingatia kanuni za uchanganyaji vyakula kwa ajili ya samaki, ili kuhakikisha wanadhibiti uchafuzi ziwani.
Luhemeja ameyasema hayo wakati akiwa jijini Mwanza katika ukaguzi wa uondoshwaji wa gugumaji jipya aina ya Salvina SSP ziwani lililoibuka hivi karibui likisababisha uhalibifu kwa vivuko.

“Wafugaji wa samaki kwa vizimba pia nao tushirkiane nao juu ya namna wanavyoingiza chakula cha samaki, tuangalie ‘quality’ (ubora) ya hivyo vyakula ili mwisho wa siku ziwa libaki kuwa salama dhidi ya uchafuzi kwaajili ya matumizi ya watu wote,”alisema Mhandisi Luhemeja.
katika hatua nyingine Luhemeja pia amesema serikali haina mashaka na shughuli za ufugaji wa vizimba lakini zipo mamlaka zinazoendelea kushughulikia kuhakikisha wanajiridhisha na aina ya vyakula wanavyopatiwa samaki hao.

“Kwahiyo lazima tuwe nao pamoja serikali, wananchi, wafugaji wa vizimba ili kuhakiki tunaliweka ziwa salama na kuwa na utatuzi wa suala hili kwa matokeo mazuri ya muda mrefu,” alisema Mhandisi Luhemeja.
Kuhusu udhibiti wa gugumaji Salvina mpaka sasa zimeondolewa tani 600 za gugu hilo hatua ambayo imesaidia kulipunguza kwa kiasi kikubwa na kudhibiti hali ya awali ya gugumaji hilo kuzuia shughuli za usafiri na usafirishaji.

Aidha alisema licha ya gugumaji hilo jipya kukabiliwa kwa sehemu kubwa, limeibuka tena gugumaji la zamani ambalo limeziba sehemu kubwa ya eneo la daraja la Kigongo-Busisi hali inayosababisha kuzuia baadhi ya shughuli za ikiuchumi ikiwemo uvuvi.
“Kwa kushirikiana na watu bode la Ziwa Victoria, NEMC pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza gugumaji jipya tumefanikiwa kuliondoa kwa asilimia kubwa lakini changamoto nyingine nay ale makubwa ya zamani ambayo yanahitaji nguvu kubwa ya ziada,” alisema.

kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amemtaka Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa kuhakikisha kifusi cha tani 600 za gugumaji jipya lililoondolewa ziwani kinaondolewa kando ya ziwa na kumwangwa katika maeneo ambayo hakitaleta athari kwa wananchi.
pia amesema Serikali imedhamiria kununua mtambo maalumu wa kusafisha ziwa victoria na mpaka sasa fedha tayari zimeshatengwa na taratibu za manunuzi zimeshaanza na muda si mrefu mtambo huo utawasili na kazi hiyo ya uvunaji wa magugu maji itaanza mara moja