Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewahimiza watu wenye ualbino nchini kutembea kifua mbele na wasiojione wanyonge kutokana na hali yao na badala yake watambue kuwa wao ni muhimu kama ilivyo kwa watu wengine.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Januari, 24 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kugawa Vifaa kinga vya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino pamoja na Uchunguzi wa Saratani ya Ngozi kwa Watu wenye Ualbino.
Amesema tukio la utoaji wa Vifaa hivyo ulioratibiwa na Manara TV kwa kushirikikana na Chama cha watu wenye ualbino ni kudhihirisha kuwa kuna ushirikiano wa dhati kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwasaidia na kuboresha maisha ya Watu wenye Ualbino nchini.
Amesisitiza kuwa watu wenye ualbino wanastahili kujiamini na kufahamu kuwa Serikali inatambua mchango wa huku akikisitiza kuwa asitokee mtu wa kuwatisha au kuhatarisha maisha ya albino kwa namna yoyote na serikali itahakikisha kwamba kundi hilo la watu linaendelea kuwa salama kama ilivyo kwa watu wengine.
Amempongeza Haji Manara na Taasisi yake ya Haji foundation kwa kujiratibu na kushiriki katika hafla hiyo ambayo imemuunganisha na watu wengine wenye ualbino jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujenga furaha kwa wengine.
“Serikali ya awamu ya sita, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha na Vifaa vingi kwa ajili ya uchunguzi katika baadhi ya Hospitali ili kuhakikisha watu wenye ualbino wanapata huduma kwa haraka na kwa ufasaha,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa vimeanzishwa vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani ya ngozi kwa Watu wenye Ualbino katika Hospitali mbalimbali ikiwemo Ocean Road, Muhimbili Bugando, KCMC, Hospitali za mikoa za Morogoro, Lindi, Mara, Iringa, Singida pamoja na Hospitali teule ya Muheza Mkoani Tanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manara Foundation, Haji Manara amewashauri watu wenye ualbino wasijinyanyapae na kwa namna yoyote ili waweze kusonga mbele kama ilivyo kwa watu wengine.
“Nikiwa mdogo sikuwahi kujielewa kama mtu mwenye ualbino na wala sikuwa kuhisi tofauti yoyote ndiyo maana nimekuwa nikifanya shughuli zote kama walikvyo wnginene, nimekuwa nikicheza mpira, nikifanya shughuli za siasa na mengine mengi.” Amesema Manara.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa jitihada za kuwekeza katika huduma za kuwawezesha watu wenye ulemavu kukabiliana na changamoto kama miale ya jua na saratani ya ngozi.
Naye Rais wa Chama cha Watu wenye ualbino, Godson Mollel amesema pamoja na changamoto kadhaa zinazowakabili wanachama, Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha na kuwajali kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila bughuda.
Ametumia jukwaa hilo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuchaguliwa na chama chake kuwa mgombe wa Urais katika Uchaguzi Mkuu ujao baadaye Oktoba, mwaka huu.
Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Tanzania Bara kuna jumla ya Watu wenye Ulemavu 5,180,095 na kati ya hao 71,631 ni Watu wenye Ualbino sawa na asilimia 0.12.