Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Viktoria ambae pia ni Mgombea wa nafasi ya makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Ezekia Wenje amewaomba wanachama wa chama hicho kutumia kauli za staha hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wao kwani kuna maisha baada ya uuchaguzi kumalizika.
Wenje ameyasema hayo hii leo wakati akitangaza nia ya kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho taifa amnapo amesema katika kipindi hiki ambacho viongozi mbalimbali wameonyesha nia ya kugombea nafasi nbalimbali wapo baadhi ya wanachama (wapambe) ambao wamekua wakiwatukana au kubeza viongozi wengine jambo ambalo sio nzuri na halikubaliki.
“Kwenye mitandao huwezi kukuta Lissu anamtukana Mbowe wanaoleta shida ni wapambe wa Lusu pamoja na wapambe wa Mbowe kwa hiyo nyie mnaonadi viongozi wetu fanyeni hivyo huku mkiweka akiba ya maneno ya kesho maana ukimtukana Lisu au Mbowe utakutana nae tu” – Wenje.
Katika hatua nyingine Wenje amesema akiwa kama mtia nia wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti yupo tayari kufanya kazi na kiongozi yoyote ambae atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho huku akisema yuko tayari kufanya majukumu yote ambayo atapangiwa.
Wenje amesema endapo atapata ridhaa ya kua makamu mwenyekiti wa chama hicho Taifa yupo tayari kwenda kusimamia maadili na nidhamu ndani ya chama hicho kwani kwa sasa chama hicho kipo katika kipindi ambacho mtu yoyote anaweza kuunda kundi sogozi na kuweka viongozi wote wa chama hicho na kuanza kulumbana jambo ambalo ni kinyume na maadili ya chama hicho.
Aidha pia amesema moja kati ya kazi kubwa ambayo ataifanya endapo atapata ridhaa ya kuwa makamu mwenyekiti ni kwenda kuinua uchumi wa chama hicho na hii ni kupitia mfumo wa kidigitali wa kusajili wanachama ( chadema Digital ) ambao utawezesha na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ndani ya chama hicho.