WENGINE 10 WAONGEZWA UFADHILI WA MASOMO NJE, IDADI YAFIKIA 60

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Serikali imeongeza nafasi nyingine 10 za Samia Scholarship Extended, na kufanya jumla ya wanafunzi 60 wa kidato cha sita kupata ufadhili wa kusoma sayansi na teknolojia za kisasa ndani na nje ya nchi.

Hatua hiyo inatokana na ushirikiano wa elimu kati ya Tanzania na Urusi, ambapo wanafunzi 10 watasoma katika Chuo Kikuu cha RUDN, Moscow wakijiunga na wenzao 50 waliokwisha chaguliwa kwenda kwenye bootcamp ya Nelson Mandela Arusha.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 13,2026 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema uchaguzi huo umefanyika kwa kuzingatia ufaulu wa juu zaidi kwa wanafunzi wa mchepuo wa PCM, PGM na PMC.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.

“Kwasababu tushachukua wakwanza mpaka Hamsini kwenda kwenye bootcamp Arusha, sasa kuanzia 51 mpaka 60 waliofanya vizuri ndiyo tunawachukua kwenda Urusi kwaajili ya kwenda kufanya bootcamp na kuja kuanza digrii ya mwakani mwezi wa Tisa,”amesema.

Kabla ya kuanza shahada, wanafunzi hao watahudhuria bootcamp ya maandalizi nchini Urusi ambapo katika kipindi hicho, Serikali ya Urusi itachangia asilimia 80 ya gharama na Samia Scholarship asilimia 20. 

“Baada ya kuanza masomo rasmi mwezi Oktoba, gharama zote zitalipwa na Serikali ya Urusi,”amesema.

Mpango huu unaonyesha dhamira ya kuandaa kizazi cha wataalamu wa Data Science, Artificial Intelligence na fani nyingine za sayansi, ili kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi wa ushindani wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *