WAZIRI MKUU WA ISRAEL, BENJAMIN NETANYAHU AMEPANDISHWA MAHAKAMANI.

Kwa mara ya kwanza Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amepanda kizimbani Jumanne kwenye kesi yake ya muda mrefu ya rushwa, huku yeye mwenyewe akidai kwamba analengwa kwa sababu ya msimamo wake mkali kuhusu usalama wa taifa.   

Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75 anakua Waziri Mkuu wa kwanza kushtakiwa akiwa  madarakani nchini Israel kwa makosa ya jinai, Wakati ambao taifa lake linakabiliana na vita vinavyoendelea Gaza na changamoto mpya za kiusalama zinazoibuka katika kanda, ikiwemo Syria.

Kwenye ushuhidi wake, Netanyahu amevishambulia vyombo vya habari vya Israel, akivilaumu kwa kuwa na msimamo wa mrengo wa kushoto na kudai kuwa vimekuwa vikimwandama kwa miaka mingi kwa sababu ya kupinga suluhisho la mataifa mawili.

Majaji wanaosimamia kesi ya Netanyahu waliamua kuwa Netanyahu atoe ushahidi mara tatu kwa wiki, jambo linalosemekana limemlazimu kugawaya muda wake kati ya mahakama na wizara ya ulinzi, ambazo ziko umbali mfupi kutoka mahakamani.

Mbele ya mahakama yenye majaji watatu, Netanyahu alisema “Nimekuwa nikisubiri miaka minane kwa ajili ya fursa hii ya kusema ukweli’’ – Netanyahu

 “Lakini mimi pia ni Waziri Mkuu, Ninaongoza nchi kupitia vita vya pande saba. Naamini kazi hizi mbili zinaweza kufanyika sambamba’’. – Netanyahu.

Waendesha mashtaka wanamtuhumu Netanyahu kwa kutoa upendeleo wa kisheria wenye thamani ya takriban dola milioni 500 kwa kampuni ya Bezeq Telecom Israel, mbali na hiyo anatuhumiwa pia kujaribu kufanikisha mpango na mmiliki wa gazeti la Yedioth Ahronoth ili kupata habari nzuri kwa kubadilishana na sheria za kupunguza ukuaji wa gazeti pinzani. Netanyahu amekana mashtaka hayo na hajakiri kosa.

huku akijitetea kwa kusema, “Kama ningehitaji habari nzuri, ningehitaji tu kuashiria msaada wangu kwa suluhisho la mataifa mawili … Kama ningechukua hatua mbili kushoto, ningesifiwa.”

Netanyahu amejitokeza akiwa mwenye tabasamu na kujiamini, huku akiwasili mahakamani saa nne asubuhi. Kesi hiyo ilihamishiwa Tel Aviv kwa sababu za kiusalama na inafanyika katika chumba cha mahakama chini ya ardhi.

Mawakili wa Netanyahu walidai kwamba uchunguzi dhidi ya Netanyahu ulikuwa na mapungufu ya msingi, wakisema kuwa “hawakuwa wakichunguza uhalifu, bali mtu binafsi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *