WAZIRI MKUU KUFANYA ZIARA MAALUM MKOANI KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, ametangaza ujio wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye anatarajiwa kufanya ziara maalum mkoani humo kuanzia Agosti 30 hadi 31, 2026. Ziara hiyo inafanyika kwa mwaliko maalum wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Baba Askofu Eusebius Zigilwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu Nchemba anatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Mpanda tangu kuanzishwa kwake. Aidha, katika kipindi cha ziara hiyo, Waziri Mkuu atashiriki katika shughuli mbalimbali zitakazoandaliwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha hatua hiyo muhimu ya kihistoria kwa Kanisa na waumini wake.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi amewaalika wananchi wote pamoja na viongozi wa taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kupokea kwa moyo wa pamoja taarifa ya ujio wa Waziri Mkuu na kushiriki katika matukio yatakayoandaliwa. Amesisitiza umuhimu wa wananchi na viongozi kuzingatia mwongozo pamoja na maelekezo ya mialiko yaliyotolewa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, huku akiwasihi kuendelea kudumisha upendo, amani na mshikamano wakati wote wa ziara hiyo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi na viongozi kuzingatia muda wa matukio yote yaliyopangwa, pamoja na kufuata maagizo yatakayotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama. Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya vyombo vinavyohusika na usalama barabarani, ili kuhakikisha shughuli za ziara hiyo zinafanyika kwa utulivu na hali ya usalama barabarani inaendelea kuwa shwari.

Akizungumza kuhusu ujio huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, amemkaribisha Waziri Mkuu pamoja na msafara wake mkoani Katavi, akieleza kuwa wananchi wako tayari kumpokea na kushiriki katika maadhimisho hayo. “Ninamkaribisha sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na msafara wote wa Waziri Mkuu,”

Kwa niaba ya wananchi wote wa Mkoa wa Katavi, ninawakaribisha sana katika Mkoa wa Katavi na katika maadhimisho ya miaka 25 ya Jubilei ya Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda,” amesema Mrindoko.

Amesema ujio wa Waziri Mkuu ni tukio muhimu kwa Mkoa wa Katavi, huku akiwahakikishia wageni na wananchi kuwa mazingira ya mkoa huo ni salama na rafiki kwa shughuli za ziara hiyo. “Katavi ni salama, Katavi ni njema na Katavi inavutia,” amesema Mkuu wa Mkoa, akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha ziara hiyo inakuwa ya amani, utulivu na mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *