
NA SAADA ALMASI-SIMIYU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa amewataka wazazi na watendaji wa Serikali kuwasimamia na kuwalinda watoto wa kike ili nao waweze kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Majaliwa ameyasema hayo wilayani busega wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa mwaka 2020/2025 kutoka kwa Mbunge wa jimbo la busega Simon Songa na kuwataka baadhi ya wazazi wanaopenda kuwashughulisha watoto wao wa kike kwa biashara katika vituo mbalimbali vya mabasi bila kujali muda wao wa masomo kuacha mara moja.

“Twende tukasimamie watoto wetu wa kike tunajua wanapenda kuwasaidia mama zao kazi za nyumbani sasa tusiwaruhusu kwenda kufanya biashara vituo vya mabasi kipindi hiki ambacho shule zinafunguliwa tujali muda wao kwani wana haki ya kwenda shule” Waziri Mkuu
Mh. Majaliwa ameongeza kwa kusema kuwa kwa sasa Serikali inatoa elimu bure kwa mtoto kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita hivyo wazazi watumie nafasi hiyo kuwasimamia na kuwahimiza kwenda shule na wanaotaka kuwakatisha watoto wa kike sheria kali zichukuliwe dhidi yao
“Mtoto wa Kitanzania anatakiwa kwenda shule na tayari Serikali imeongezwa hadi kidato cha sita elimu bure wewe kwa nini hutaki kumpeleka mtoto shule? Na anayebainika kumkatisha mtoto wa kike masomo yake sheria zipo zifuatwe” waziri mkuu
Akiwasilisha utekelezaji wa mradi wa maji jimboni hapo ambao kwa sasa upo katika asilimia 78 za utekelezaji mbunge wa jimbo hilo simon Songa amesema kuwa hadi kufikia mwakani wananchi wote wa jimbo hilo watakuwa wamepata huduma hiyo
“kwa sasa tuko katika asilimia 78 za upatikanaji wa maji ambayo ni mradi kutoka maji ya ziwa viktoria ninawaahidi kwamba hadi kufikia mwakani tutakuwa tumekamilisha upatiikanaji wa maji kwa asilimia 100”
Nae waziri wa maji Jumaa Aweso amesema kuwa kukamilika kwa mradi wa maji mkoani Simiyu wenye thamani ya zaidi ya bilioni 400 ni jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha mwanamke anatuliwa ndoo kichwani
“serikali yetu haitaki kuona mwanamke anateseka kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji na ndiyo maana imetekeleza mradi huu ili kila mwanamke atuliwe ndoo kichwani” Waziri Aweso