Waziri Bashe atoa siku 7 kwa kampuni ya vodisel kulipa deni la halmashauri ya ushetu

Serikali imetoa siku saba kwa kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya VODISEL kulipa fedha za ushuru wa tumbaku inayodaiwa na halmashauri ya Ushetu kiasi cha shilingi Milioni 362.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa kilimo Hussen Bashe wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya ushetu katika Kijiji cha Mbika kata ya Ushetu halmashauri ya ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Katika hatua nyingine Waziri Bashe amesema kuwa katika msimu wa kilimo 2024/2025 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa mabani ya kudumu ya kuchomea tumbaku na kwamba kila kampuni itakayopewa leseni ya kununua tumbaku mwaka huu inawajibu wa kutenga shilingi 40 kwa kila kilo atakayonunua kwa ajili ya kujenga mabani ya wakulima.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani ameiomba Serikali kupitia Waziri wa Kilimo kumpunguzia madeni mkulima hasa madeni ya miti na kuiomba serikali kuwa deni hilo libebewe na kampuni zinazonunua tumbaku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *