WAZEE WA KIMILA WASIFU UTULIVU MGODINI MARA

Uongozi wa Baraza la Wazee wa mila, wa koo 12 wilayani Tarime mkoani Mara, umeeleza kuridhishwa na hali ya utulivu inayoendelea kuimarika katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, kufuatia kupungua kwa matukio ya uvamizi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya vijana kutoka vijiji vinavyozunguka eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa kando ya kongamano lililofanyika mjini Tarime, lililolenga kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Akizungumza na Tovuti hii, Katibu wa Baraza la wazee wa mila wa koo 12 wilayani Tarime Mwita Nyasibora,amesema kuwa mabadiliko hayo yanatokana na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa vijana kuhusu umuhimu wa uwekezaji na fursa zilizopo ndani ya sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wilaya ya Tarime ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Meja Edward Gowele, amesema hali ya uvamizi iliyokuwa ikishuhudiwa hapo awali imepungua kwa kiasi kikubwa, hali inayochangia kuimarika kwa usalama katika eneo hilo.

“Tangu mwaka 2020 kwa siku vijana waliokuwa wanavamia huo mgodi walikuwa si chini ya 100,lakini mpaka tunavyoongeza hivi sasa ni hawazidi 7 na hii ni kwa sababu wananchi wameshaona faida za uwekezaji katika sekta ya madini”.Amesema Mkuu wa wilaya ya Tarime.

Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfan Haule, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, amewataka wawekezaji katika sekta ya madini kuendelea kutoa ajira zaidi kwa vijana, hususan ajira zisizohitaji ujuzi mkubwa ili kuongeza ushiriki wa wananchi wa maeneo husika.

Aidha Mratibu wa kongamano hilo, Deus Bugaywa, amesisitiza umuhimu wa majukwaa ya majadiliano kama hayo katika kujenga uelewa na kuimarisha mahusiano kati ya jamii na wawekezaji.

Kupungua kwa matukio ya uvamizi katika mgodi wa North Mara ni ishara ya mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya serikali, jamii na wawekezaji katika kuhakikisha kunakuwepo mazingira salama ya uwekezaji huku wananchi wakinufaika na rasilimali zilizopo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *