Wazazi wamehimizwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanapokuwa nyumbani, ili kusaidia kukuza uwezo wao kitaaluma na kujenga msingi bora wa elimu, badala ya kutegemea Walimu pekee, katika jukumu hilo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa shule ya Shekinah Pre & Primary School, Obadia Mwambapa wakati wa siku maalumu ya kufunga shule, ambapo amesema ushirikiano kati ya wazazi na walimu ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na elimu bora.

Amesema wazazi wanapaswa kutenga muda wa kufuatilia masomo ya watoto wao, kujua changamoto wanazokutana nazo na kushirikiana na walimu katika kutafuta suluhisho.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Juliana Sabrere amesema ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la pamoja kati ya walimu na wazazi, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kulinda maadili mema ya watoto na kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye malezi yanayozingatia misingi ya heshima, uwajibikaji na nidhamu.
Amesema malezi bora ya watoto yanahitaji ushiriki wa pande zote mbili, kwa kuwa mtoto anahitaji uangalizi na mwongozo akiwa shuleni na nyumbani.

Aidha, amewataka wazazi na walimu kuwa karibu na watoto, kuwasikiliza na kuwasaidia kutambua mambo mema na mabaya ili kujenga kizazi bora cha sasa na cha baadaye.
Kwa upande wao, mwalimu pamoja na mzazi wa wanafunzi waliokuwepo katika hafla hiyo, wameunga mkono umuhimu wa malezi shirikishi, wakisisitiza kuwa mafanikio ya mtoto hayawezi kutegemea upande mmoja pekee. Wamesema ushirikiano wa karibu kati ya mzazi na mwalimu husaidia kufuatilia maendeleo ya mtoto kitaaluma, kitabia na kijamii.
Wamewataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu kwa kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya watoto wao na pia kufuatilia mwenendo wao wanapokuwa nyumbani, huku walimu wakiendelea kutoa elimu na mwongozo unaohitajika shuleni.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha watoto wa Shekinah Pre & Primary School wanapata elimu bora sambamba na malezi yanayowajenga kuwa na maadili mema, nidhamu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya sasa na baadae.


