Na Tryphone Odace – Kigoma.
Wazazi na walezi katika Kijiji cha Matyazo, Kata ya Kalinzi, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wamekubaliana kuendelea kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Matyazo, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya uongozi wa shule na wazazi, ambapo washiriki walijadili umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wanapokuwa shuleni.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa kikao hicho, Mkuu wa Shule ya Sekondari Matyazo, Mwl. Elias Pius Soza, alisema lengo la kikao lilikuwa kuhamasisha wazazi na walezi kuendelea kushiriki katika utoaji wa chakula kwa wanafunzi ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Upatikanaji wa chakula shuleni ni muhimu katika kuwawezesha wanafunzi kuwa na anakuwa na utayari wa kujifunza na kutumia muda mwingi zaidi katika masomo yao, huku ukisaidia pia kupunguza utoro.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Matyazo, Kateksita Joseph Kalla, alisema makubaliano ya kuchangia chakula shuleni yanapaswa kutekelezwa kwa wakati ili kuwezesha shule kufikia malengo iliyojiwekea, hasa katika kuboresha taaluma na ustawi wa wanafunzi.
Alieleza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, walezi, walimu na uongozi wa shule ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kufanya vizuri katika masomo yao.

“Unajua hawa ni watoto wetu na ni jukumu letu kushirikiana kuhakikisha wanapata chakula shule itasaidia kuwa na utulivu wakiwa darasani lakini tunaongeza morali ya mwanafunzi kupenda shule na utoro utakuwa umeisha na ufaulu watafaulu vizuri.” Alisema Kalla.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi waliohudhuria kikao hicho, akiwemo Abasi Mayeye, Winfrida Christopher na Khalifa Zuberi, waliahidi kuendelea kushirikiana na walimu na uongozi wa shule katika michango mbalimbali yenye lengo la kuboresha elimu na ustawi wa wanafunzi.

Walisema wataendelea kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, wakisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ushiriki wa wazazi katika kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia na kusaidia watoto wao kufikia malengo yao ya kielimu.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuongeza muda wa kujifunza na hatimaye kuchangia katika kuimarika kwa kiwango cha ufaulu katika Shule ya Sekondari Matyazo.


