Na Pascal Tuliano – Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amewataka Wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari pamoja na Watendaji wa Kata kuendelea kuwahamasisha Wananchi hususan wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya Wanafunzi akibainisha kuwa mchango huo ni muhimu.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya hali ya lishe kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Wella amesema Watendaji wa Kata ni wasimamizi wa viashiria vya lishe katika maeneo yao huku akifafanua kuwa moja ya viashiria hivyo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja anapokuwa shuleni, hususan kwa wanafunzi wasiokuwa wa bweni.

Katika kikao hicho, imebainika kuwa bado wapo wazazi wanaokosa utayari wa kuchangia chakula shuleni kwa watoto wao. Mhe. Wella amesema hali hiyo inahitaji kuendeleza juhudi za kutoa elimu na hamasa kwa wazazi, ili waweze kuchangia bila mashaka.
Aidha, Wella amewakumbusha watendaji kuwa kuchangia chakula cha wanafunzi ni takwa la kisheria na mzazi mwenye uwezo anayeshindwa kufanya hivyo kwa makusudi anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ndogo za halmashauri au hata sheria mama za nchi na amesisitiza kuwa elimu kwa wazazi inapaswa kuzingatia pia wajibu huo wa kisheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa maeneo ambayo Halmashauri haikufanya vizuri kwenye viashiria vya lishe japo ni machache yatafanyiwa kazi kwa usimamizi wa karibu, huku akiahidi kuwa mwaka wa fedha 2025/2026 watendaji wake watahakikisha viashiria vyote vinatimizwa ipasavyo.