Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amewataka wazazi kuhakikisha wanachangia chakula kwa watoto wao wakiwa shuleni, ili kuboresha uelewa wao darasani.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ikomwa, DC Wella amesema kuwa watoto hukaa muda mrefu shuleni, hivyo kukosa chakula kunachangia kushuka kwa uwezo wa kuelewa masomo.

“Mtoto anapokuwa na njaa hawezi kufuatilia vizuri masomo darasani. Ni muhimu kila mzazi akahakikisha mtoto wake anapata angalau mlo mmoja akiwa shuleni,” amesema DC Wella.
Aidha, amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi muhimu wa afya na maendeleo ya mtoto, na kwamba ushiriki wa wazazi katika suala la chakula mashuleni utasaidia kuinua kiwango cha elimu katika jamii.

Wananchi wa Kata ya Ikomwa wamehimizwa kushirikiana na viongozi wa elimu na serikali za mitaa ili kuhakikisha mpango wa chakula mashuleni unatekelezwa kwa ufanisi.


