WAWAKILISHI WA TABORA SHIMISEMITA WAHIMIZWA NIDHAMU, MAADILI WAKATI WA MASHINDANO

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima amewataka watumishi watakaoiwakilisha Manispaa hiyo katika Michezo ya Kitaifa ya Watumishi wa Halmashauri mbalimbali nchini (SHIMISEMITA), kuwa na nidhamu na kuzingatia maadili wakati wote wa mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika jijini Mbeya mwezi Agosti 2026.

Akizungumza wakati wa kutoa hamasa na nasaha kwa timu hiyo, Dkt. Pima amesema ushiriki wao katika michezo hiyo ni sehemu ya kuwakilisha Manispaa ya Tabora, hivyo amewataka kutumia nafasi hiyo kwa kuonyesha uwezo, nidhamu na mshikamano katika kipindi chote cha mashindano.

Dkt. Pima pia amewahimiza watumishi hao kupambana kwa bidii na kutumia uwezo wao wote kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo hiyo, akisisitiza kuwa Halmashauri imewaamini na kuwateua wao kuwa wawakilishi wa Manispaa katika mashindano hayo ya kitaifa.

Aidha, amewataka kuwa mabalozi wazuri wa Manispaa ya Tabora kwa kuzingatia nidhamu, kuheshimu washiriki wengine pamoja na kuzingatia taratibu na kanuni zitakazotolewa na waandaaji wa mashindano hayo.

Kwa upande wao, wawakilishi hao wa Manispaa ya Tabora wapo katika maandalizi ya mwisho kuelekea mashindano hayo, huku wakitarajiwa kuanza safari ya kwenda jijini Mbeya mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kushiriki SHIMISEMITA 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *