Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga amewasimamisha kazi Watumishi watatu wa Kituo cha Afya Kabuku walioshiriki kumpatia huduma Mama mjamzito aliyepoteza Maisha pamoja na kichanga chake.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Novemba 11 2023 ikidaiwa kuwa marehemu alikosa huduma ya upasuaji baada ya kushindwa kulipa kiasi cha shilingi Laki moja na elfu hamsini alizotakiwa kutoa kwa ajili ya huduma hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema amepokea kwa masikitiko habari za kifo cha mama huyo kinachoelezwa kuwa chanzo ni uzembe wa Watumishi wa Kituo hicho.
Ummy amesema tayari Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ametuma Timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa inayojumuisha Madaktari bingwa wawili (Daktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi na Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi ) ili kufanya uchunguzi wa tukio hili.