WATUMISHI, WAFANYABIASHARA WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA UBADHIRIFU GEITA

Na Ibrahim Rojala – Geita.

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita, imewafikisha mahakamani Watumishi kumi na wafanyabiashara wanne kwa ubadhirifu wa fedha za mirathi zaidi ya milioni 260.

Ubadhirifu huo, ulifanyika katika akaunti ya mirathi ya Mahakama kuu Masijala ndogo ya Geita, ambapo watumishi hao waliwalipa wanufaika wanane wasio na madai yoyote ya mirathi mahakamani, kwa lengo la kurudisha fedha hizo (Kick Back), kwa watumishi hao na kwa wenza wao, kupitia miamala ya kibenki na mitandao ya simu kinyume na taratibu.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Taasisi hiyo Aprili 30, 2026 watumishi waliohusika na ubadhirifu huo  ni hakimu mahakama ya mwanzo Nyankumbu, Veronica Japhet Mwasenga, Afisa hesabu mkuu, Bulemo Yuda Mswaga, Msaidizi wa hesabu, Mercy Geoffrey Magezi, Mhasibu Baldo Donatus Kafene, Msaidizi wa Kumbukumbu, Emma Emmanuel Matabaro na dereva, William John Mbwambo kutoka mahakama ya hakimu mkazi Geita.

Aidha kwa mujibu wa taarifa hiyo, watumishi hao walitekeleza  ubadhirifu huo kwa kushirikiana na watumishi kutoka idara zingine za serikali ambao ni tabibu wa halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Upendo Aloyce Rugohe, mtumishi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar Es Salaam (DUCE), Felix  Casmiry Swaty, Mhaidrojia wa Wizara ya Maji Dodoma, Salim Issa Lyimo na Diwani wa Kata ya Majengo, Monduli Arusha, Mgema Magembe Julius.

Wahusika wengine ni wafanyabiashara wanne ambao ni Amani Idd Abdallah, Erick Albert Chitumbi, Michael Samson Chanzi na David George Mrope.

Kufuatia matukio hayo, TAKUKURU mkoa wa Geita baada ya kupata vibali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani Aprili 30, 2026 na kufunguliwa mashauri matano katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Geita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *