Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka watumishi wa sekta ya maji kuhakikisha wanawafuata wateja katika maeneo yao ya huduma, ili kuharakisha na kurahisisha huduma kwa Watanzania.
Aweso ametoa agizo hilo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji kusini mwa Dar es Salaam unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA).

Aweso ameshuhudia baadhi ya watumishi wa kitengo cha huduma kwa wateja Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jiji la Dar es salaam wakitoa huduma katika viwanja vya wazi eneo la Bangulo.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya wiki ya maji ambayo kilele chake ni Machi 22 yakitarajiwa kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Aweso amesema hiyo ndiyo tafsiri ya utumishi wa umma ambapo mteja anasikilizwa na kuhudumiwa katika mazingira yake.
Awali akipata maelezo ya mradi huo Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema mradi huo umetekekezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 36.8 na umekamilika kwa asilimia 100.

Amesema mradi huo uko katika majaribio ya awali yatakayo kamilika mwishoni mwa mwezi huu na unatarajia kuhudumia zaidi ya wakazi 4500 wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa pwani.
Aidha, mradi huo utakuwa suluhisho la huduma ya majisafi katika maeneo ya kusini mwa jiji la Dar es Salaam ambayo yamekuwa na changamoto kwa muda mrefu.

Katika ziara hiyo Waziri Aweso amezungumza na wananchi katika eneo la Kifuru na kuwahakikshia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anapambana kuhakikisha tatizo la huduma ya maji jiji la Dar es salaam linaisha kabisa.