WATUMISHI BRELA WASISITIZWA UADILIFU NA NIDHAMU KATIKA KAZI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amewataka watumishi wa taasisi hiyo kuzingatia maadili na kuweka nidhamu katika utendaji kazi, ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.

Nyaisa ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu na watumishi wote wa BRELA kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukumbushana majukumu, kusikiliza changamoto za kiutendaji na kuzitatua pamoja na kuwapongeza wafanyakazi bora na kuwaaga watumishi walio staafu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa akifafanua jambo wakati wa kikao maalumu na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa lengo la kukumbushana majukumu na kusikiliza changamoto na kuzitatua kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

“Napenda kuwasisitiza sana suala la nidhamu ya kazi, tujenge utamaduni wa kuheshimu nafasi tulizonazo na tuwe waadilifu mahala pa kazi ili hata ukienda taasisi nyingine nje ya BRELA waone kweli umejifunza kazi na unaiweza kufanya kwa ufanisi,” alisema Nyaisa.

Aliongeza kuwa, kila mmoja atambue wajibu wake na kuutekeleza, na kuwataka wafanyakazi hao watambue kwamba juhudi za mfanyakazi mmoja mmoja ndizo zinazompa nafasi Afisa Mtendaji Mkuu kuonekana kuwa anafanya kazi na kuipa sifa Taasisi kwa ujumla.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi hodari kutoka Idara na Vitengo vya taasisi baada ya kuwapongeza katika hafla iliyofanyika baada ya kikao na wafanyakazi kwa lengo la kukumbushana majukumu na kusikiliza changamoto na kuzitatua kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Aidha, Nyaisa amesema ataendelea kufanyia maboresho ya kiutendaji changamoto zilizopo na kuwataka wafanyakazi kuendelea kuwa wavumilivu wakati misingi ya maboresho ikiendelea kuwekwa kwa ajili ya watumishi wote.

Kikao hicho kilifuatiwa na hafla ya kuwapongeza wafanyakazi bora na hodari waliofanya vizuri kwa mwaka 2023/2024 ambao walitunukiwa vyeti na zawadi kwa wafanyakazi bora huku mfanyakazi Hodari wa Taasisi akipata cheti na TZS. Milioni tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *