Watumishi 3 wa afya wasimamishwa, 26 kuchunguzwa

Ujumbe wa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu umewasimamisha kazi watumishi watatu kupisha uchunguzi na wengine 26 kutoka idara mbalimbali wakiendelea kufanyiwa uchunguzi kwa kukwamisha utoaji Huduma kwa wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo.

Ujumbe huo ukiongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel umefanya maamuzi wakati wa ziara yake ya siku moja kufuatilia maelekezo ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu juu ya kero kwa wananchi wa Tanga kutopata Huduma nzuri za afya.

Dkt. Mollel amesema watumishi watatu waliosimamishwa kazi ni Daktari Bingwa wa Mifupa, Mtaalam wa Usingiz na Muuguzi wa Chumba cha Upasuaji.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi katika idara zote za Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo na watumishi wengine 26 wanaendelea kuchunguzwa zaidi”. Ameeleza Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel ametoa onya kali kwa madaktari wote nchini wenye tabia za kutoa rufaa kwa wagonjwa bila sababu za msingi za matibabu kutoka kwenye Hospitali za Serikali na kuwapelekea kwenye hospitali binafsi.

Aidha, amesema wamiliki wa hospitali binafsi wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo katika kuendesha hospitali zao kwani yeyote atakayebainika kuwarubuni madaktari wa hospitali za Serikali kutoa rufaa bila sababu ya msingi ya kimatibabu watachukuliwa hatua za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *