Watu zaidi ya 600 kushiriki jukwaa la  ushirika Shinyanga

Zaidi ya watu 600 wanatarajiwa kushiriki katika Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoa wa Shinyanga linalotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 21 hadi 22 litakaloshirikisha viongozi wa vyama vya Ushirika,Taasisi wasimamizi ikiwemo Ushirika chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Chuo kikuu cha ushirika Moshi,Shirika la Ukaguzi pamoja na wadau wengine wa Ushirika ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.

Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga Bi.Hilda Boniface  amebainisha hayo Machi 20,2024  na kueleza kwamba jukwaa hilo litakalofanyika katika Cha Ushirika Moshi,Taasisi ya Elimu ya  Biashara Kizumbi Manispaa ya Shinyanga na kueleza kwamba malengo ya jukwaa hilo ni kuwawezesha wadau na wasimamizi kukaa meza moja na kujadili mambo yote yanayohusiana na ushirika.

“Wadau watajadili mafanikio mbalimbali waliyoyapata,changamoto zilizojitokeza kwa  mwaka mzima tangu tulipokutana,lakini pia na fursa kama zipo basi ni wakati muafaka wa kuweza kuambizana ili kuona kila mmoja kuona ni kwa namna gani anavyoweza akatumia nafasi ya jukwaa hilo ili kujiimarisha zaidi au namna anavyoweza kuhamasisha chama chake cha ushirika mahali anakotoka”amefafanua Mrajis Hilda

Aidha ameeleza kwamba kupitia jukwaa hilo wakulima wataweza kukutana na wadau wanaoujihusisha na uuzaji wa pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na pembejeo za ruzuku na njia ya kawaida pamoja na wadau wengine hali itakayowawezesha wadau wa kilimo na sekta nyingine kukutana na wataalamu wenye uwezo wa kutoa majibu ya changamoto zao pamoja na changamoto za ushirikia.

Miongoni mwa mada zinazotarajiwa kuwasilishwa kupitia jukwaa hilo ni pamoja na ujasiriamali ili kuwawezesha wakulima kulima kwa tija,kisasa na kuendesha kilimo biashara,uendelezaji wa fedha zinazotokana na kilimo zitakazowasaidia  katika misimu ya kilimo inayofuata pamoja na elimu ya usimamizi wa fedha na matumizi bora ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo.

“Tunataka tumpe mkulima elimu sasa ili awe mjasiriamali baada ya kuunganishwa na soko bora,akapata malipo yake mazuri asiishie kuzitapanya zile pesa mpaka zikaisha tunataka tumpe elimu sasa ili awe mjasiriamali,tunataka kesho tutoke kwenye kilimo cha kujikimu tuwahamasishe watu wetu waweze kulima kilimo cha kibiashara”Amesemea Hilda.

Sambamba na hilo kupitia Jukwaa hilo wahudhuriaji watapata fursa ya kupata elimu ya usimamizi wa fedha na vyama vya akiba na mikopo ili kuhakikisha baada ya kukamilika kwake washiriki wote wanakuwa na elimu ya kutosha inayohusu masuala ya fedha.

Katika kuhakikisha jukwaa hilo linakuwa na tija kwa watakaohudhuria licha ya kukutanishwa na kuwa na vyama vya ushirika litawezesha kupatikana kwa utatuzi wa changamoto mbalimbali kutokana na uwepo vyama vya akiba na mikopo,vyama vya ushirika vya madini na ufugaji  ng’ombe na vyama vingine kwa lengo la kuimarisha ushirika na kumfanya mwanaushirika na jamii kwa ujumla kujikwamua katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *