Watu 143 wamefariki nchini Brazil baada ya mvua kubwa kunyesha katika jimbo la Rio Grande do Sul kwa zaidi ya wiki mbili,Mamlaka nchini Brazil imesema watu wengine 125 hawajulikani waliko katika jimbo hilo la kusini mwa Brazil huku viwango vya maji kwenye mito vikiripotiwa kupanda.
Idara ya hali ya hewa imesema mvua inayoendelea kunyesha inatia wasiwasi mnamo Jumamosi ya Mei 11 serikali ilitenga Sh315 bilioni ili kusaidia katika kukabiliana na janga hilo ambalo hadi sasa limewalazimisha watu 538,000 kuyahama makazi yao.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema serikali kuu itajenga upya miundomsingi yote iliyoharibiwa na mvua katika jimbo hilo la Rio Grande do Sul,kwa upande wake, Rais Joe Biden wa Amerika amesema utawala wake utatuma msaada kwa waathiriwa wa mafuriko katika nchi hiyo.
“Tunatuma rambirambi zetu kwa wale waliopoteza jamaa zao nchini Brazil. Kando na hayo, tunawapongeza mashirika na watu binafsi waliojitolea kuwaokoa waathiriwa wa janga hilo. Tutatuma msaada nchini humo ili kuwasaidia waathiriwa,” Biden alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Mvua zaidi ilinyesha Jumapili na Jumatatu ya wiki hii na tangu mvua kuanza kunyesha katika nchi hiyo wiki mbili zilizopita, serikali inasema iko macho na kwamba inajaribu kupunguza athari ya mafuriko kwa kuhakikisha kuwa kiwango cha maji hakipandi katika Ziwa Guaiba, karibu na mji mkuu wa Porto Alegre.
Kando na kusababisha maafa, mafuriko hayo pia yameporomosha majengo na kusomba miundombinu na hivi sasa baadhi ya waathiriwa kwa sasa wanaishi shuleni, kambi za wakimbizi na wengine kupewa makazi ya muda serikali ikijaribi kutafuta suluhu ya kudumu.