Taarifa kutoka Idara ya Polisi Nchini Kenya zinasema miili ya watu wasiopungua 13 imeopolewa kutoka maeneo tofauti ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi baada mafuriko ya kutisha kulikumba taifa hilo la Afrika Mashariki.
Serikali imeunda kikosi cha dharura kushughulikia janga hilo na wakati huohuo Idara ya Polisi imeendelea na juhudi za uokozi kwa ambao nyumba zao zimefunikwa na maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Kati ya hiyo,miili 11 imepatikana eneo la Mathare, mmoja Kibera na mwingine Kayole,maeneo ambayo yanapatikana katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi na inahofiwa kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka japo juhudi za uokozi zinaendelea na maelfu wameachwa bila makazi baada ya mafuriko kuathiri nyumba na baadhi ya barabara hazipitiki.
Kwa mujibu wa mkuu wa polisi kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei, vikosi vya pamoja kutoka idara mbailmbali vinashirikiana kutoa usaidizi wa kila aina katika Kipindi ambacho Rais wa Taifa hilo William Ruto ameshauri wakazi wa maeneo yaliyo kwenye kingo za mito kuhama.