WATU 1,275 WAMEPOTEZA MAISHA KWA AJALI ZA BARABARANI – BASHUNGWA

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Imeelezwa kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Aprili, 2025, watu waliopoteza maisha kutokana na ajali ni 1,275 ikilinganishwa na idadi ya watu 1,408 waliokufa kwa kipindi kama hicho cha mwaka 2023/24. 

Hayo yamebainishwa leo Mei 26,2025 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na kuongeza kuwa idadi ya watu waliokufa kwa ajali za barabarani imepungua kwa watu 133 sawa na asilimia 9.4. 

“Watu 2,278 walijeruhiwa kutokana na ajali kwa kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Aprili 2025, ikilinganishwa na watu 2,166 waliojeruhiwa kwa kipindi kama hicho katika mwaka 2023/24. Hili ni ongezeko la watu 112 sawa na asilimia 5.2,” amesema. 

Aidha, ameongeza kuwa Jeshi la Polisi katika kudhibiti matukio ya ajali barabarani imeandaa mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kutoa ushauri kwa sekta ya umma na sekta binafsi katika kujenga barabara salama na kuboresha alama na taa za barabarani, kujenga madaraja ya waenda kwa miguu na vidhibiti mwendo kama matuta.

“Pia, tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari ili kuhakikisha yanafuata viwango vya usalama na kufuata kanuni, sheria na taratibu za usalama barabarani,”ameongeza. 

Mbali na hayo amesema wataendelea kuchukua na kusimamia sheria na adhabu kali kwa madereva wasiozingatia sheria za barabarani kama vile kuendesha kwa kasi, ulevi na matumizi ya simu wakati wa kuendesha vyombo vya moto, sambamba na kuendelea kufanya doria za masafa marefu (High way Patrol).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *