Watu 100 Wahisiwa Kuugua Homa ya Ini Ushetu

Na William Bundala,Ushetu

Wananchi katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya afya vinavyotoa huduma ya vipimo vya ugonjwa wa homa ya ini ambavyo ni Ukune,hospitali ya wilaya Ushetu na kituo cha afya Bulungwa ili  kufanya vipimo vya  ugonjwa huo ambao ni hatari kwa sasa  unaoelezwa kuwa kasi yake ya maambukizi inazidi kasi ya maambukizi ya upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI).

Wito huo umetolewa Agosti 29,2024 na Mganga mkuu wa halmshauri ya Ushetu Dkt. Athuman Matindo wakati akizungumza na jambo Fm ofisini kando ya kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika hii leo.

 Dkt.Matindo amesema kuwa miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa ya manjano,kukojoa mkojo mweusi  na mwili kukosa nguvu joto kuongezeka na kuyataja makundi yanayoweza kuambukizwa ugonjwa huo kuwa ni waraibu wa dawa za kulevya na wanaofanyabiashara ya ngono.

Awali akichangia hoja katika kikao cha baraza la madiwani,diwani wa kata ya Bulungwa katika halmashauri hiyo Kalwani Mteganoni amesema kuwa katika kata yake watu watatu wa familia moja wanahisiwa kuwa na ugonjwa wa homa ya ini na kuiomba serikali kutoa chanjo kwa jamii inayowazunguka,wakati huo huo mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu ametoa maagizo kwa mganga mkuu na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuchukua hatua stahiki dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa halmashauri ya Ushetu Dkt Athuman Matindo amesema kuwa kuanzia Januari hadi Agosti 2024 jumla ya wananchi 100 wamepimwa na kuhisiwa kuwa na vimelea vya ugonjwa wa homa ya ini na kupatiwa matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *